Jumatatu, 27 Novemba 2017

MMILIKI WA SHULE YA SEKONDARI SCOLASTICA APIGWA PINGU

Ama kweli sheria ni msumeno,pichani Edward Shayo,mmoja wa wamiliki wa shule ya Sekondari Binafsi ya Scolastica iliyopo Himo mkoani Kilimanjaro,akiwa amepigwa pingu muda mfupi baada ya kutoka kwenye chumba cha mahabusu kilichopo mahakama ya hakimu mkazi,Shayo na wenzake wawili wamesomewa shitaka la mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo,Humphrey Makundi.
Jengo la mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ambako washitakiwa wa mauaji ya mwanafunzi Humphrey Makundi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Binafsi ya Scolastica iliyopo mji mdogo wa Himo Mkoani Kilimanjaro walisomewa shitaka la mauaji ya mwanafunzi huyo.

Hili ndilo kaburi ambalo linadaiwa kuzikwa  mwili wa marehemu Humphrey Makundi mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Binafsi ya Scolastica iliyopo katika mji mdogo wa Himo Mkoani Kilimanjaro anayedaiwa kuuawa na mlinzi wa shule hiyo Novemba 6 mwaka huu na mwili wake kutupwa mto Wona mita 300 kutoka shuleni hapo,mwili huo ulizikwa makaburi ya Karanga Mjini Moshi kabla ya kufukuliwa Novemba 17 baada ya mahakama ya hakimu mkazi kutoa kibali cha kuufukua



WATUHUMIWA MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SHULE YA SCOLASTICA WAPANDISHWA KIZIMBANI




Na Charles Ndagulla,Moshi

WATU  watatu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwanafunzi Humphrey makundi(16) wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Scolastica iliyopo katika mji mdogo wa Himo,leo wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na shitaka moja la mauaji.

Washitakiwa hao ni pamoja na mmoja wa wakurugenzi wa shule hiyo,Edrwad Shayo,Mwalimu wa shule hiyo Laban Nabiswa pamoja na mlinzi wa shule hiyo,Hamis Chacha.

Walisomewa shitaka hilo na wakili wa serikali Cassim Nasri akisaidiwa na wakili wa Serikali Faygrace Sadallah mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya Julieth Mawole .

Akisoma hati ya mashitaka,wakili Nasri alidai kuwa,mnamo Novemba 6 mwaka huu huko maeneo ya  Himo wilaya ya Moshi,washitakiwa kwa pamoja walimuua kwa makusudi mtu mmoja aitwaye Humphrey Makundi.

Baada ya kusomewa shitaka hilo,washitakiwa hao hawkautakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji hadi mahakama kuu.

Washitakiwa walipelekwa mahabusu kwenye gereza kuu la mkoa,Karanga na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Decemba nane mwaka huu huku vilio vikitawala mara baada ya washitakiwa hao kusomewa shitaka lao.

Mshitakiwa wa pili na mmoja wa wamiliki wa shule hiyo,Edward Shayo alishindwa kujizuia na kumwaga chozi  muda mfupi  baada ya kutoka mahakamani huku akiwapa wosia ndugu zake akiwataka wamwombee kwani anaamini mungu yupo na atatenda muujiza.

Shayo alifikishwa mahakamani hapo peke yake  saa 5:39 akiwa ndani ya gari la polisi lenye namba za usajili T367 CAF aina ya Toyota landCruser akitokea Hospital ya Rufaa ya KCMC ambako amekuwa akipatiwa matibabu tangu kukamatwa kwake na alipanda kizimbani pamoja na wenzake saa 7 :11 mchana .

DONDOO ZA TUKIO LILIVYOKUWA

1.Novemba 6 mwaka huu mwanafunzi huyo alidaiwa kutoweka shuleni hapo

2.Novemba 10 mwaka huu mwili wake uliokotwa ndani ya Mto Wona na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa,Mawenzi

3.Novemba 12 mwili wa marehemu ulizikwa na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga baada ya kutojitokeza ndugu wa kuutambua 

4.Novemba 17 mwaka huu mahakama ya hakimu mkazi mjini moshi ilitoa kibali cha mwili huo kufukuliwa baada ya ndugu wa marehemu kubaini kuwa mwili uliozikwa katika makaburi hayo ni wa mtoto wao.

MWILI WAFANYIWA UCHUNGUZI

Mwili wa marehemu Humphrey ulifanyiwa uchunguzi na madaktari katika Hospital ya rufaa ya KCMC na kushuhudiwa na Baba mzazi wa marehemu na katika uchunguzi huo,ikibainika marehemu alikatwa na kitu chenye ncha kali kiunoni,mgongoni,kwenye mapaja na mbavu mbili zilivunjika.

Baba mzazi huyo akawaeleza wanahabari kuwa kulingana na majibu ya uchunguzi huo ni ukweli ulio wazi kuwa,mwanaye aliuawa na kwamba kifo chake kinatia shaka na kuvitaka vyombo vya uchunguzi kuwasaka wahusika wa mauaji ya mtoto wake mpendwa.

Jumapili, 26 Novemba 2017

MAAJABU YA PANZI HIFADHI YA MSITU WA ASILI MILIMA YA ULUGURU

Pichani ni panzi mwenye alama ya bendera ya Taifa anayepatikana ndani ya Hifadhi ya msitu wa Asili uliopo milima ya Ulunguru mkoani Morogoro(Picha na Sitta Tuma)
 Pichani ni panzi mwenye alama namba tisa mgogoni pia akiwa na miguu mitatu,naye ni moja ya maajabu yanayopatikana ndani ya hifadhi ya msitu wa Asili uliopo milima ya  Uluguru mkoani Morogoro.(picha na Sitta Tuma)

MAZINGIRA:MOYO UNAOHITAJI ULINZI THABITI



Na Sitta Tumma, Mwanza
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinaoathirika na mabadiliko ya tabianchi, yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
 
Athari za mabadiriko haya yanasababisha hasara ya upotevu wa mali, maisha ya watu, mimea na viumbe vingine hai na visivyo hai, kama vile udongo.

Zaidi ya watu milioni 200 duniani kote wanaathirika na ukame, mafuriko, vimbunga, matetemeko, moto, milipuko ya mabomu na majanga mengine.

Aidha kuongezeka kwa majanga kumeongeza kasi ya watu kuathirika kiuchumi, pamoja na kuongeza idadi ya watu masikini duniani.

Kwa mtu asiyeelewa maana ya mabadiriko ya tabianchi, ni mtiririko wa mfumo wa mabadiliko ya  hali ya hewa.

Yanayochukua muda mrefu au mfupi.Husababisha hali mbaya za hewa, ama uchache wa hali inayohitajika au wingi wa hali isiyohitajika.
Husababsisha madhara kwa jamii na nchi kwa ujumla. Ndiyo!

Tatizo hili limekuwa miongoni mwa ajenda kuu za Umoja wa Mataifa (UN) na Jumuiya ya kimataifa  kwa mwaka 2014.

Dunia imejielekeza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ili kuishinda vita hii lazima kila mtu abebe jukumu la kutunza mazingira yanayomzunguka.

Kuwepo kwa majanga haya duniani kunatokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu, zinazoathiri mfumo mzima wa hali ya hewa na mazingira.

Baadhi ya shughuli hizo ni ukataji miti ovyo, utiririshaji maji machafu, uvuvi wa kutumia sumu, ujenzi na uendeshaji viwanda vinavyochafua mazingira.

Umwagaji ovyo wa kemikali, madini na matumizi mabaya ya ardhi. Vichocheo vingine ni uchomaji moto misitu.

Mabadiriko ya tabianchi pia husababisha mafuriko, ukame na magonjwa dhidi ya wananchi na mimea!

Kwa zaidi ya miaka 50, hali ya hewa duniani imekuwa ikibadilika, kutokana na kuongezeka gesi chafu zinazozalishwa na mvuke wa maji, methane na  kaboni  dayoksaidi.
                    Uhifadhi Misitu

Kulingana na hayo, Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) imeweka mikakati ya kulinda mazingira na utunzaji wa misitu nchini.

Hifadhi ya Msitu wa Asili ya Milima ya Uluguru, iliyopo Mkoa wa Morogoro, ni moyo unaohitaji uangalizi madhubuti kwa faida ya jamii na maendeleo ya taifa.

Hifadhi hii inatakiwa kulindwa na kutunzwa na jamii yenyewe ya vijiji 62 vinavyozunguka msitu huo.

Tunapozungumzia Msitu wa Uluguru, tunagusa uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Msitu huu ni hazina ya maendeleo na hifadhi ya mazingira, si tu kwa Mkoa wa Morogoro bali ukanda wote wa Pwani na Dar es Salaam.

Juma James na Halima Musa, ni wakazi wa Mkoa wa Morogoro, wanasema uwapo wa msitu huo unawasaidia kupata hewa safi.

Mbali na hilo, wanasema unawasaidia pia kupata mvua kwa ajili ya kikimo, ingawa wanakiri hivi sasa hali ya hewa imebadirika kuliko awali.

"Lakini pia watalii wanapokuja kwenye Misitu ya Uluguru wananunua bidhaa zetu. Wengine wanalala Morogoro na kuongeza pato la wafanyabiashara.

"Mimi mwenyewe ingawa sijawahi kuingia kwenye misitu hii, lakini nafarijika sana kuona namna uoto wa asili unavyovutia," anasema Husna Ali (42) mkazi wa Morogoro.
              Panzi wa ajabu

Moja ya vivutio vya kitalii vilivyomo kwenye Hifadhi ya Uluguru, ni panzi mwenye rangi ya bendera ya Taifa la Tanzania. Ndiyo. Yupo!

Akizungumza na timu ya waandishi wa habari za mazingira, waliotembelea hivi karibuni hifadhi hii, Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Misitu ya Uluguru, Mohamed Borry, anasema panzi huyo hapatikani kokote duniani, isipokuwa kwenye msitu huo.

Timu hiyo ya wanahabari ilizuru eneo hilo, wakati wa mafunzo ya siku tano dhidi yao, yaliyoandaliwa na Muungano wa Vilab vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweeden kupitia Shirika lake la Maendeleo (SIDA).

"Yupo pia panzi mwingine yeye ana alama ya namba tisa mgongoni mwake. Huyu anaonekana Desemba 9 (siku nchi ilipopata uhuru wake-mwaka 1961).

"Uwapo wa msitu huu na viumbe hivi, inatulazimu sisi jamii tuendelee kutunza mazingira yanayotuunguka," anasema Borry na kuongeza:

"Mazingira ni uhai. Bila kutunza mazingira jamii ndiyo inayoathirika zaidi na uchafuzi huo. Kwa sababu kutakuwa na ukame, magonjwa, kukosa chakula na maji."

Mhifadhi Borry hapa anazitaja vivutio vingine vya kitalii, vilivyomo kwenye Hifadhi hiyo ya Uluguru kuwa ni vyura mwenye mguu mmoja, miwili na mitatu.
 
Kwa mujibu wa ofisa huyo, wapo pia vinyonga wenye pembe moja, mbili na tatu.
Kwamba uwapo wa viumbe hao unaonesha umuhimu wa jamii kutunza mazingira.

"Faida ya kutunza mazingira katika Msitu huu wa Uluguru, watu 151,000 wanaotoka vijiji 62 vinavyozunguka hifadhi hii watanufaika kiuchumi.

"Kwa sababu viumbe na uoto huu ni kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

"Hivyo watalii wanapokuja wananunua bidhaa za wananchi na wenyeji kunufaika kuwapandisha milimani watalii," anasema Borry.
                  
                                                Utafiti


Utafiti wa Wakala wa Huduma ya Misitu nchini (TFS) unasema kwamba, heka 400,000 ya misitu inapotea kila mwaka kutokana na ukataji kuni, ujenzi, uchomaji misitu nakadhalika.

Vivyo hivyo, utafiti wa mwaka 2013 unasema jumla ya tani milioni moja za mkaa hutumika kila mwaka. Hii ni kutokana na ukosefu wa ajira.

Wataalamu wa masuala ya mazingira wanasema, asilimia 40 ya ardhi inayofaa kwa kilimo imeharibiwa vibaya, kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Kwamba uchafuzi huo unaofanywa na binadamu, unachangia mmomonyoko wa udongo jambo linaloathiri pia kilimo.

Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 pamoja na Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 zinazuia uharibifu wa misitu na uchomaji moto, ambapo imeainisha pia adhabu kwa waharibifu.

Pia, Sheria ya Mazingira No. 20 ya mwaka 2004, na ile ya Usimamizi wa Railimali ya Maji Na. 11 ya mwaka 2009, zinazuia pia uchafuzi wa maingira.

Kulingana na hayo, Sheria ya Maji inasema wazi kwamba, uchafuzi wa maji nikosa la jinai, na mtu au kiwanda hakitakiwi kutiririsha maji machafu bila kuwa na kibali cha Bodi ya Taifa ya Maji.

Wazir wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba, amekuwa akisisitiza kitu mtu nchini kutunza mazingira.

Waziri Makamba anataka kuona Sheri ya Mazingira inatekelezwa kwa vitendo, ikiwamo wachafuzi wa mazingira kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs) unaosimamiwa na UN duniani, unasisitiza kila nchi na raia wake kutunza mazingira.

Katika taarifa iliyotolewa mwaka jana na UN inasema kuwa, takribani watu milioni 700 wanaishi chini ya mstari wa umasikini duniani.

Mwandishi mkongwe wa habari za mazingira nchini, Deodatus Mfugale, yeye anaeleza kuchukizwa na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na jamii.

Mfugale anasema, uchafuzi wa mazingira una athari kubwa katika maisha ya binadamu na viumbe wengine.

Unasababisha magonjwa, vifo, ukame na kudhorota kwa afya za watu walioathiriwa na tatizo hilo.

"Binadamu ndiye anayeathirika zaidi na athari za uchafuzi wa mazingira. Kila mtu awajibike kulinda na kutunza mazingira.

"Sheria zipo, zisimamiwe kikamikifu kudhibiti uchafuzi wa mazingira Tanzania," anasema Mfugale.

Kufuatia hayo yatupasa kila mtu ayalinde na kutunza mazingira yanayomzunguka. Mazingira ni 'Moyo' unaohitaji uangalizi mzuri.

Jumamosi, 25 Novemba 2017

VIPIMO VYA DNA VYAKWAMISHA MAZISHI YA MWANAFUNZI WA SCLOLASTICA HIGH SCHOOL

Askari wakishirikiana na ndugu wa marehemu Humphrey Makundi kufukua kaburi ulimozikwa mwili huo katika makaburi ya Karanga mjini Moshi hivi karibuni baada ya mahakama ya hakimu mkazi mjini Moshi kutoa kibali cha kuufukua mwili huo kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi.


Baba mzazi wa marehemu Humphrey makundi ,Jackson Makundi(katikati)akijadili jambo na ndugu zake wakati zoezi la kuufukua mwili wa mwanaye likiendelea katika makaburi ya Karanga mjini Moshi hivi karibuni. 



Na Charles Ndagulla,Moshi

MAZISHI  ya mwanafunzi,Humphrey Makundi(16) wa shule ya Sekondari ya Scolastica iliyopo katika mji mdogo wa Himo anayedaiwa kupigwa na kitu chenye ncha kali,yamekwama kufanyika jumamosi hii.

Kukwama kwa mazishi hayo kunatokana na kuchelewa kutoka kwa majibu ya vipimo vya vinasaba(DNA)vilivyopelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali na sasa mazishi hayo yatafanyika wiki ijayo.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki hii mjini hapa,Baba mzazi wa marehmu,Jackson Makundi alisema kuwa wanatarajia kupata majibu ya vipimo hivyo wiki ijayo na baada ya kutoka kwa majibu hayo,tararibu za mazishi zitafanyika mapema iwezekanavyo.

“Tunaomba uchunguzi ufanyike haraka na majibu ya vipimo yatoke haraka ili niweze kumzika kwa heshima mtoto wangu,kwakweli ameteseka sana”,alisema makundi katika mkutano wake na vyombo vya habari.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika shule hiyo,anadaiwa kutoweka shuleni hapo asubuhi ya Novemba saba na mwili wake kupatikana Novemba 10 ukiwa ndnai ya mto Wona mita 300 kutoka shule hapo.

Mwili huo unadaiwa kukutwa na majeraha kichwani hali inayodhihirika kuwa kabla ya kifo chake marehemu aliteswa kwa kupigwa na kitu kizito kilichopasua fuvu lake.

Baba mzazi wa marehemu alisema katika mkutano wake na wanahabari kuwa,kwa mujibu wa taarifa aliyopewa na daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo,mwanye alipigwa na kitu chenye ncha kali na kupasua fuvu na kukana taarifa zinazoenezwa kuwa alikufa kwa maji.

Hadi sasa jeshi la polisi linawashilia zaidi ya watu 11 kwa mahojiano akiwamo mmiliki wa shule hiyo,Edward Shayo wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo ambayo yameutikisa mji wa Himo na mkoa mzima wa Kilimanjaro.

Mauji hayo pia yamelaaniwa na baadhi ya wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule mbali mbali za bweni huku wakitilia shaka usalama wa watoto wao na kuzitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na kuwafikisha mahakamani watakaobainika kutenda unyama huo.

Wengine wanaoshikiwa yumo mlinzi wa shule hiyo anayedaiwa kumpiga na kitu kizito marehemu,wamo daktari katika hopsital ya mkoa,mawenzi wanaodaiwa kufanya udanganyifu kuhusu umri wa marehemu na kutoa kibali cha kuuzika mwili huo chap chap.



 

HIFADHI YA MAZINGIRA ASILI AMANI TANGA NA HISTORIA LUKUKI



Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani ndiyo hifadhi kongwe kuliko hifadhi asilia zote nchini, Hifadhi hii ilitangazwa rasmi kwenye gazeti la Serikali mwaka 1997. Hifadhi hii ipo katika Wilaya za Muheza na Korogwe umbali wa kilomita 64 kutoka Jijini Tanga.

Amani yenye ukubwa wa hekta 8,380 ni moja kati ya maeneo ya mfano yaliyohifadhiwa vizuri nchini kwa kutumia mfumo wa Uhifadhi Shirikishi baina ya Serikali na wananchi wanaoishi na kuzunguka katika hifadhi hiyo.

Akizungumza na Ndagullablog, Afisa Misitu Mkuu wa Hifadhi hiyo, Angyelile Sousa alisema, Serikali kupitia Wakala wake wa Huduma za Misitu (TFS) imewekeana Makubaliano ya kuhifadhi Msitu huo na vijiji 21 vinavyozunguka hifadhi hiyo. Vijiji vinne kati ya hivyo ambavyo ni Shebomeza, Mlesa, Chemka na Mikwinini vimo ndani ya Hifadhi hiyo Asilia.

Sousa alisema katika mfumo huo kila kijiji kimeunda kamati ya uhifadhi wa mazingira ambazo zinashirikiana kwa karibu na uongozi wa hifadhi hiyo kwenye shughuli za uhifadhi ikiwemo ulinzi wa rasilimali zilizomo.

Alisema kuwa makubaliano hayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa wananchi wa vijiji hivyo wameelimishwa na kuuelewa umuhimu wa hifadhi hiyo ambayo ina faida kubwa kwao, kwa Serikali na kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga.

Aliongeza kuwa mfumo huo umesaidia kuimarisha uhifadhi katika Msitu huo ambapo matukio ya moto yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa ikiwa na pamoja na shughuli za uharibifu wa mazingira kwa ujumla.

Akielezea faida za hifadhi hiyo alisema, Amani ni chanzo kikuu cha Maji yanayotumika katika Jiji la Tanga ambapo vyanzo vyake vinapeleka maji katika mto Zigi unaopeleka maji hayo Jijini humo. Vijiji vyote 21 vinavyozunguka hifadhi hiyo pia vinanufaika na maji hayo.

Alisema kuwa faida nyingine inayopatikana katika hifadhi hiyo ikiwa ni sehemu ya makubaliano kwenye uhifadhi shirikishi ni mchango wa asilimia 20 ya mapato yanayotokana na utalii ambayo yanatolewa kwa vijiji 21 vinavyopakana na hifadhi hiyo kwa ajili ya kusaidia katika shughuli za maendeleo za vijiji hivyo.

“Katika sehemu ya makubaliano hayo wananchi wa vijiji jirani wanaruhusiwa kuokota kuni kavu zinazopatikana katika hifadhi hiyo, matunda, mbogamboga pamoja na dawa za miti shamba. Wananchi hao wanaruhusiwa kuingia hifadhini kwa umbali wa mita 100 kutoka maeneo yao ya vijiji kwa ajili ya shughuli hizo” alisema Sousa.

Aliongeza kuwa watu binafsi pia wananufaika na hifadhi hiyo kwa kuwekeza katika mahoteli yanayowapatia kipato. Wananchi pia wanaotembeza watalii katika hifadhi hiyo wananufaika na ajira ambapo huchukua asilimia 60 ya mapato ya kutembeza watalii (Tour Guiding Fees), asilimia 20 ikibaki hifadhini na asilimia 20 nyingine ikienda kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.

Akizungumzia vivutio mbalimbali vilivyomo katika hifadhi hiyo, Sousa alisema kuna vivutio vingi vya utalii vilivyohifadhiwa vizuri ikiwemo Misitu ya Asili na Wanyama mbalimbali kama vile Kima wa Bluu (Blue Monkey), Mbega Weupe na Weusi (Black and White Collabus), Nyoka, vinyonga pembe tatu (Three Hornes Chamelleon), vipepeo na ndege wa aina mbali mbali ambao baadhi yao husafiri umbali mrefu kutoka barani ulaya kwa ajili ya kukimbia baridi kali na kuzaliana katika hifadhi hiyo.

“Vivutio vingine vilivyopo katika hifadhi hii ni Maporomoko ya Maji (Water Falls) ambayo ni Derema, Chemka, Ndola na Pacha. Pia kuna vivutio vya Vilele vya Milima (viewpoints) kama Kiganga, Ngua, Makanya, Mbomole na Kilimahewa. Ukiwa katika vilele hivyo unaweza kuona Mji wa Korogwe na Jiji la Tanga kwa juu” alisema.

Mbali na vivutio hivyo, alisema kivutio kingine ambacho ni cha kipekee katika hifadhi hiyo ni aina ya Ua linaloitwa “Saintpaulia” ambalo lina rangi ya Zambarau “Violeth Color”, Ua hilo pia linatumika kama nembo ya hifadhi hiyo. Upekee wa Ua hilo ni kwamba likipandwa sehemu nyingine yeyote duniani hubadilika rangi yake ya asili, Tafiti mbalimbali zimefanywa ikiwemo kujaribiwa kupandwa nchini Ujerumani na kutoa majibu hayo hayo.

Pamoja na vivutio hivyo kivutio kingine katika hifadhi hiyo ni mashine ya kusagia unga iliyokuwa ikitumia nishati ya nguvu ya kusukumwa na maji miaka 1986 katika kijiji cha Kisiwani na mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati hiyo hiyo iliyotumiwa na Wakoloni wa Kijerumani katika Kijiji cha Chemka.

Akizungumzia aina za utalii katika hifadhi hiyo alisema, upo Utalii wa Picha (Photography), Utalii wa Kutizama Ndege (Bird Watching), Utalii wa Kuangalia viumbe hai Usiku (Night Watching), Utalii wa Kiutafiti (Reseach Tourism), Utalii wa kiutamaduni (Cultural Tourism) na Utalii wa Kutembea na Kupanda Milima.

“Kwa upande wa gharama za kutembelea hifadhi ya Amani kama kiingilio kwa Mtalii mmoja kutoka nje ya nchi ni Dola 10 za Kimarekani na Mtanzania ni Shilingi10,000. Kwa upande wa gharama za watembeza watalii wa nje ni dola 15 za Kimarekani” alisema.

Nae Afisa Misitu wa Hifadhi hiyo, Isack Bob Matunda akizungumzia idadi ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo na mapato yaliyopatikana alisema “Mwaka wa fedha 2015/16 jumla ya watalii 545 walitembelea hifadhi hii na jumla ya mapato yote yaliyopatikana ni shilingi milioni 50. Aidha, mwaka huu wa fedha 2016/17 mwezi Julai-Agosti jumla ya watalii 121 wameshatembelea hifadhi hii na mapato ambayo yameshapatikana ni shilingi milioni 7.3”.

Akielezea changamoto za uhifadhi, Afisa Misitu Mkuu wa Hifadhi hiyo, Angyelile Sousa alisema zipo changamoto kidogo ikiwemo uchimbaji wa madini kwenye vyanzo vya maji, uharibifu mdogo wa misitu ikiwa ni pamoja na uchomaji moto katika ukanda wa chini na miundombinu mibovu ya barabara.